May 16, 2017 03:53 UTC
  • Watu sita wauawa katika shambulio la Boko Haram katika mji wa Maiduguri

Watu wasiopungua 6 wanaripotiwa kuuawa kufuatia shambulio la kundi la kigaidi la Boko Haram kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Ripoti za awali zinasema kuwa, wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram wamewaua wakulima sita kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika ambao walikuwa katika shughuli zao za kawaida. Mauaji hayo yametokea jirani na mji wa Maiduguri makao makuu ya jimbo la Borno.

Baada ya shambulio hilo, jeshi la Nigeria liliwafuatilia wanachama hao na kufanikiwa kumuangamiza mmoja kati yao. Shambulio hilo la Boko Haram linajiri siku chache tu baada ya kundi hilo kutoa mkanda wa video wa mmoja wa wanachama wake akitishia kwamba, kundi lao litafanya mashambulio dhidi ya mji mkuu wa Nigeria Abuja.

Wanachama wa Boko Haram

Kundi la Boko Haram lilianzisha mashambulizi dhidi ya maeneo ya umma na taasisi za serikali huko kaskazkini mwa Nigeria mwaka 2009 na baadaye mwaka 2015 likapanua mashambulizi hayo hadi katika nchi za Chad, Cameroon na Niger.

Zaidi ya watu elfu 20 wameuwa kufikia sasa katika mashambulizi hayo na wengine zaidi ya milioni mbili wamelazimika kuwa wakimbizi.

Serikali ya Nigeria inayoongozwa na Rais Muhammadu Buhari imeendelea kukosolewa vikali kutokana na kile kinachoelezwa kuwa, kushindwa serikali yake kukabiliana na kundi hilo ambalo limetenda jinai nyingi. 

Tags