UN: Ubakaji unatumiwa kama mbinu ya ugaidi Somalia, Nigeria
Umoja wa Mataifa umesema uhalifu wa kijinsia unatumiwa na magaidi kama moja ya mbinu zao katika nchi za Somalia, Nigeria na Mali.
Amina Mohammed, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameliambia Baraza la Usalama la umoja huo kuwa, magenge ya kigaidi kama vile Boko Haram, al-Shabaab na Daesh (ISIS) yameshadidisha uhalifu wa kijinsia dhidi ya wanawake na hususan waliowateka nyara.
Amesema mbali na kuwabaka wanawake hao, magaidi hao baadhi ya nyakati hufanya magendo ya mateka wao wa kike ili kupata pesa za kuendeleza harakati zao.
Mbali na nchi hizo za Afrika, mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa amesema genge la kigaidi na kitakfiri la Daesh linatumia mbinu hiyo ya kuwadhalilisha wanawake katika nchi za Syria na Yemen.
Naye Adama Dieng, Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya uhalifu wa kijinsia katika migogoro ameliambia Baraza la Usalama la UN kuwa, magaidi wanawabaka wanawake na kuutumia uozo huo kama chombo cha udhalilishaji, adhabu na kuwatia fedheha.
Itakumbukwa kuwa, baadhi ya wanafunzi wa kike wa Shule ya Upili ya Chibok ya Nigeria waliokuwa wametekwa nyara na genge la kitakfiri la Boko Haram, walirejea nyumbani wakiwa wajawazito na baadhi yao wakiwa na watoto.