Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ataka kurejeshwa utulivu nchini Libya
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amezitaka pande zote zinazopigana kusini mwa Libya kufanya juhudi za kurejesha amani na utulivu katika eneo hilo.
Antonio Guterres sambamba na kuonyesha wasiwasi mkubwa ulionao Umoja wa Mataifa kutokana na kushadidi mapigano katika kambi ya kijeshi ya Brak al-Shat kusini mwa Libya ameyataka makundi yanyohusika katika mapigano hayo yapige moyo konde na kurejesha amani na utulivu katika maeneo hayo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, kuendelea ukosefu wa amani na utulivu nchini Libya ni ishara kwamba, nguvu za kijeshi haziwezi kuwa chaguo mwafaka la kuinasua nchi hiyo katika mgogoro iliyokwama ndani yake.
Antonio Guterres amesisitiza kwamba, ili kuiondoa Libya na mgogoro inaokabiliwa nao kuna haja ya kuweko mazungumzo ya kisiasa.
Kwa akali watu 141 wameripotiwa kupoteza maisha katika shambulio lililoilenga kambi ya jeshi huko kusini mwa Libya, mapigano ambayo yametajwa kuwa, wimbi jipya la machafuko katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Machafuko nchini humo yaliibuka mwaka 2011, baada ya wananchi wa taifa hilo la kaskazini mwa Afrika kuiondoa madarakani serikali ya Kanali Muammar Gaddafi, kiongozi wa zamani wa nchi hiyo kwa kushirikiana na Marekani na baadhi ya mataifa ya Ulaya na ya eneo. Tangu wakati huo hadi leo, nchi hiyo imeendelea kushuhudia machafuko ambayo yamezidi kuiharibu.