Ndege za Misri zashambulia maficho ya magaidi nchini Libya
Jeshi la Anga la Misri limefanya mashambulizi katika maficho ya magaidi ndani ya ardhi ya Libya baada ya watu wenye silaha kushambulia mabasi mawili yaliyokuwa na Wakristo mkoani al Minya.
Press TV imeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, ndege za Misri zimefanya mashambulizi mara sita katika maeneo yanayotumiwa na magaidi kutoa mafunzo katika mji wa Derna wa kaskazini mashariki mwa Libya.
Taarifa ya jeshi la Misri imesema kuwa, ndege za nchi hiyo zimefanya mashambulizi hayo baada ya kuwa na yakini kwamba magaidi walioshambulia mabasi ya Wakristo katika mkoa wa al Minya wa Misri, walitokea kwenye kambi hiyo ya magaidi.
Wakati huo huo jeshi la taifa la Libya linaloongozwa na Jenerali Khalifa Haftar limetoa tamko na kusema kuwa, lilishirikiana na jeshi la Misri katika mashambulizi hayo ya Derna.
Rais Abdul Fattah el Sisi wa Misri alisema jana usiku kwamba nchi yake itaendelea kushambulia maficho ya magaidi popote yalipo, iwe ni ndani au nje ya ardhi ya Misri.
Misri imesema kuwa, magaidi waliokimbia mapigano nchini Syria wamerejea nchini Misri na kuhatarisha usalama wa nchi hiyo.
Watu 28 wameuawa na wengine 24 kujeruhiwa katika shambulio la jana Ijumaa lililofanywa na watu 10 wenye silaha dhidi ya mabasi mawili yaliyokuwa na Wakristo katika mkoa wa al Minya nchini Misri.