Ikhwanul Muslimin: Shambulizi la Misri nchini Libya litazidisha uhasama wa nchi mbili
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i29754-ikhwanul_muslimin_shambulizi_la_misri_nchini_libya_litazidisha_uhasama_wa_nchi_mbili
Kundi la Ikhwanul Muslimin lililopigwa marufuku nchini Misri, limelaani mashambulizi ya nchi hiyo huko Libya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 29, 2017 09:27 UTC
  • Ikhwanul Muslimin: Shambulizi la Misri nchini Libya litazidisha uhasama wa nchi mbili

Kundi la Ikhwanul Muslimin lililopigwa marufuku nchini Misri, limelaani mashambulizi ya nchi hiyo huko Libya.

Taarifa iliyotolewa na kundi hilo imesema kuwa, shambulizi hilo la ndege za jeshi la Misri huko Libya, limetokana na kushindwa serikali ya Cairo kuwashika wahusika wa shambulizi la mji wa Minya. Kadhalika ripoti hiyo ya Ikhwanul Muslimin imeongeza kuwa, hatua hiyo ya Misri dhidi ya Libya itaongeza uhasama na nchi hiyo jirani.

Ndege za Misri zikiwa katika anga ya Libya kuwashambulia magaidi

Harakati hiyo imesema kuwa shambulio la jeshi la nchi hiyo nchini Libya litauletea maslahi utawala wa Kizayuni kwa ajili ya kulifanya eneo lote kuwa dhaifu na lililogawika. Aidha imewataka Wamisri kuungana pamoja na kuchukua hatua yenye lengo la kuiokoa Misri kwa kile ilichokiita kuwa ni kupenda kujitanua Rais Abdel Fattah el-Sisi wa nchi hiyo. Itakumbukwa kuwa jeshi la anga la Misri lilitekeleza mashambuli siku za Ijuma na Jumamosi katika mji wa Derna, mashariki mwa Libya kwa madai kuwa, mji huo unatumiwa na magaidi wenye mafungamano na Daesh (ISIS) katika kuratibu mashambulizi nchini humo.

Wanachama wa kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) nchini Libya

Muda baada ya shambulizi hilo nchini Libya jeshi la taifa la Libya linaloongozwa na Jenerali Khalifa Haftar lilitoa tamko na kusema kuwa, lilishirikiana na jeshi la Misri katika mashambulizi hayo ya Derna. Watu 28 waliuawa na wengine 24 kujeruhiwa katika shambulio la siku ya Ijumaa lililofanywa na magaidi 10 wenye silaha dhidi ya mabasi mawili yaliyokuwa yamewabeba Wakristo katika mkoa wa al Minya nchini Misri.