Miili 7 ya wahajiri wa Kiafrika yapatikana ndani ya lori Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i30070-miili_7_ya_wahajiri_wa_kiafrika_yapatikana_ndani_ya_lori_libya
Wahajiri saba wa Kiafrika wamepoteza maisha baada ya kukosa hewa wakiwa ndani ya lori lenye jokofu kwa muda wa siku mbili katika pwani ya Libya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 05, 2017 09:36 UTC
  • Miili 7 ya wahajiri wa Kiafrika yapatikana ndani ya lori Libya

Wahajiri saba wa Kiafrika wamepoteza maisha baada ya kukosa hewa wakiwa ndani ya lori lenye jokofu kwa muda wa siku mbili katika pwani ya Libya.

Adel Mostafa, afisa wa Idara ya Kupambana na Wahamiaji Haramu wa Libya amewaambia waandishi wa habari mjini Tripoli kuwa, wahajiri wengine 28 wameokolewa kwenye lori hilo lililopatikana limetelekezwa na wafanya magendo ya wahajiri katika mji wa Garabulli, yapata kilomita 50 mashariki mwa Tripoli.

Mashuhuda wanasema walisikia sauti za vilio kutoka kwenye lori hilo na kwamba dereva wake alikimbia baada ya watu wasiojulikana kuanza kulifytaulia risasi kwenye magurudumu.

Wahajiri wa Kiafrika wakielekea Ulaya kwa boti ya plastiki

Wiki iliyopita, wahajiri 44 ambao wengi wao ni kutoka nchi za magharibi mwa Afrika walifariki dunia kwa kiu kaskazini mwa Niger baada ya lori walilokuwa wakisafiria kuharibika katikati ya jangwa.

Kwa mujibu wa Shirika la Wahajiri Duniani IOM, watu wanaofanya biashara haramu ya magendo ya wahajiri wanatengeneza faida ya dola bilioni 35 za Marekani kwa mwaka.

Aghalabu ya wahajiri ambao kutokana na sababu za kiuchumi huamua kuziacha nchi zao kwa tamaa ya kwenda kutafuta kazi na maisha mazuri barani Ulaya, wanatokea katika nchi za Nigeria, Eritrea, Somalia, Sudan, Gambia, Senegal, Mali, Morocco na Tunisia.