Jun 08, 2017 07:56 UTC
  • Boko Haram washambulia Waislamu wakila futari Nigeria

Makumi ya wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram wameshambulia vijiji vilivyoko kando kando ya mji wa Maiduguri, kaskazini mashariki mwa Nigeria wakati ambapo Waislamu wa mji huo walikuwa majumbani kwao wakila futari.

Mashuhuda wanasema milio ya risasi na miripuko ilisikika jana wakati wa magharibi viungani mwa mji huo, baada ya magaidi hao kuuvamia na kuzusha taharuki.

Msemaji wa Jeshi la Nigeria, Brigedia Jenerali Sani Uthman hata hivyo amesema uvamizi huo umedhibitiwa na kuwataka wakazi wa mji huo kutokuwa na wasi wasi.

Afisa huyo wa ngazi za juu wa jeshi la Nigeria hajatoa maelezo yoyote kuhusu wahanga wa mashambulizi hayo ya jana jioni, kwa upande wa raia au wanachama wa genge hilo la kitakfiri. 

Wanachama wa genge la kigaidi la Boko Haram

Mwishoni mwa mwezi uliopita, watu wanane waliuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa katika wimbi la hujuma za kigaidi lililoutikisa mji huo wa Maiduguri.

Kundi la Boko Haram lilianzisha mashambulizi dhidi ya maeneo ya umma na taasisi za serikali huko kaskazkini mwa Nigeria mwaka 2009 na baadaye mwaka 2015 likapanua mashambulizi hayo hadi katika nchi za Chad, Cameroon na Niger. Zaidi ya watu elfu 20 wameuawa kufikia sasa katika mashambulizi hayo na wengine zaidi ya milioni mbili na laki saba wamelazimika kuwa wakimbizi.

Tags