Umoja wa Ulaya wasisitiza kuendelea kushirikiana na DRC
Umoja wa Ulaya umesisitiza kuwa, utaendelea kushirikiana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kwamba, vikwazo vya umoja huo dhidi ya baadhi ya viongozi wa nchi hiyo havitaathiri ushirikiano wa pande mbili.
Hayo yameelezwa na Bart Ouvry balozi wa Umoja wa Ulaya katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambaye amesisitiza kuwa, vikwazo vya umoja huo kwa baadhi ya viongozi wa Kinshasa havina taathira katika mwenendo wa ushirikiano kati ya pande hizo mbili.
Akizungumza mjini Kinshasa balozi na mwakilishi huyo wa Umoja wa Ulaya katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amesema kuwa, ushirikiano wa umoja huo ni wa kudumu na wa kuendelea kwa muda mrefu.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, Léonard She Okitundu Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo alisema hivi karibuni akilihutubia bunge la nchi hiyo kwamba, endapo Umoja wa Ulaya hautafuta vikwazo ulivyowawekea maafisa tisa wa nchi hiyo, basi Kinshasa nayo itachukua hatua mkabala na hiyo.
Kulingana na Umoja huo wa Ulaya waliolengwa na vikwazo hivyo vinavyojumuisha kufungiwa kwa mali zao na kuzuiwa kusafiri wanashikilia nyadhfa za juu katika uongozi na vyombo vya usalama. Maafisa hao wa serikali wanatuhumiwa kuhusika na mauaji katika makabiliano baina ya vyombo vya usalama na waandamanaji waliokuwa wanampinga Rais Joseph Kabila mwaka jana, ambapo watu zaidi ya 50 walifariki dunia.