Umoja wa Mataifa waitaka DRC kupunguza wanajeshi wake mkoani Kasai
Mshauri maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amezihimiza mamlaka katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kupunguza wanajeshi wake katika mkoa wa Kasai, baada ya kuibuka vurugu mbaya za mauaji katika miezi ya hivi karibuni.
Watu zaidi ya 3,300 wameuawa katika miezi minane ya kuongezeka kwa machafuko katika mkoa wa Kasai katikati mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Umoja wa Mataifa siku ya Ijumaa ulisema kuwa, utatuma timu ya wataalamu kuchunguza ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu katika mkoa huo.
Adama Dieng amewaambia waandishi wa habari mjini Kishasa kuwa ni muhimu kupunguza wanajeshi wa serikali mkoani Kasai na kutoa kipaumbele kwa mazungumzo baina ya pande zote mbili zinazohusika katika mzozo.

Hayo yanajiri huku Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ikiendelea kushuhudia harakati za makundi ya waasi hususan mashariki mwa nchi hiyo ambazo zimesababisha mauaji, ukosefu wa amani na raia wengi kuyakimbia makazi yao wakihofia usalama wao.
Mkoa wa Kasai ulikumbwa na ghasia na vurugu baada ya kuuawa Kamwina Nsapu kiongozi wa kikabila ambaye alikuwa akipambana na serikali ya Rais Joseph Kabila.
Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa juzi lilipasisha azimio la kutuma wataalamu wa kimataifa katika eneo la Kasai la katikati mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa ajili ya kuchunguza mapigano na machafuko yaliyotokea katika mji huo.