Algeria: Tutatoa ushirikiano wowote kusaidia kutekelezwa makubaliano ya kisiasa Libya
Serikali ya Algeria imeuhakikishia Umoja wa Mataifa kufanya juhudi zozote zinazohitajika kwa ajili ya kufanikisha utekelezwaji wa makubaliano ya kisiasa nchini Libya.
Abdul Aziz bin Ali Sharif, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Algeria ameyasema hayo alipokutana na Ghassan Salamé, mjumbe maalumu mpya wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya ambapo pamoja na mambo mengine alisisitiza kuwa, Algiers itafanya juhudi za kila upande ikiwa ni pamoja na kuunga mkono mazungumzo, kusaidia kufikiwa maridhiano ya kitaifa na pia kulindwa umoja wa kitaifa wa Libya.
Kadhalika bin Ali Sharif aliongeza kuwa, Algeria imekuwa ikifanya juhudi hizo kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa na serikali ya umoja wa kitaifa nchini Libya ikiwa ni katika kutekeleza makubaliano ya kisiasa yaliyotiwa saini tarehe 17 Disemba 2015 katika mji wa Skhirat, magharibi mwa Morocco. Makubaliano hayo ya kisiasa ya Disemba mwaka 2015 yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa, ndiyo yaliyopelekea kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa nchini Libya.
Serikali hiyo ya umoja wa kitaifa ina jukumu la kuhitimisha mvutano kati ya serikali mbili hasimu za Tripoli na Tobruk sambamba na kurejesha usalama na amani ndani ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.