Jul 06, 2017 04:07 UTC
  • Serikali Afrika Kusini kuchukua udhibiti wa ardhi bila kutoa fidia

Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini amesema kuna pendekezo la kuiwezesha serikali ya nchi hiyo kuchukua udhibiti wa ardhi pasina kulipa fidia kwa wamiliki wa ardhi hiyo.

Akizungumza Jumatano, Zuma amesema chama tawala cha ANC kimependekeza katika kongamano lake la sera kuwa, serikali iwe na uwezo wa kuchukua udhibiti wa ardhi pasina kulipa fidia wakati kunapokuwa na dharura.

Suala la umiliki wa ardhi linatazamiwa kujadiliwa kwa kina kabla ya kongamano la mwezi Desemba la ANC wakati mrithi wa Zuma atakapoteuliwa.

Naibu wa Rais wa Afrika Kusini, Cyrila Ramaphosa na mkuu wa zamani wa Tume ya Umoja wa Afrika, Nkosazana Dlamini-Zuma, ambaye aliwahi kuwa mke wa rais Zuma, wanatajwa kuwa wanaongoza katika kuwania nafasi hiyo.

Nkosazana Dlamini-Zuma

Atakayechaguliwa kama mwenyekiti wa ANC atakuwa na nafasi kubwa ya  kuwa rais wa nchi hiyo baada ya kipindi cha Zuma kumalizika mapema mwaka 2018.  Uchumi wa Afrika Kusini umedorora na kiwango cha ukosefu wa ajira ni asilimia 28 huku nchi hiyo ikikumbwa na mivutano ya kisiasa.

Dlamini-Zuma katika kampeni zake amekuwa akisisitiza ulazima wa Wazalendo Waafrika waliowengi kupewa umiliki wa ardhi ambazo zimekuwa zikidhibitiwa na makaburu Wazungu waliowachache nchini humo kwa muda mrefu. Anasisitiza kuwa serikali inapaswa kuchukua ardhi hizo pasina kuwalipa fidia makaburi waliozinyakua kutoka kwa wazalendo.  

Tags