Mlipuko wa bomu wauwa watu 5 na kujeruhi 18 Benghazi, Libya
Watu kadhaa wameuawa na wengine kujeruhiwa baada ya bomu kulipuka kando ya barabara inayotumiwa na vikosi vya jeshi la Libya katika mji wa Benghazi, mashariki mwa nchi hiyo.
Duru za kijeshi za Libya zimeripoti leo kuwa, watu wasiopungua 5 wameaga dunia na wengine 18 wamejeruhiwa baada ya bomu kulipuka karibu na Hospitali ya Jamhuri katika eneo la Sabiri katika mji wa Benghazi.
Duru hizo zimeeleza kuwa, makundi ya kigaidi yamehusika na utegaji mabomu kando ya barabara zinazotumiwa na vikosi vya jeshi la Libya. Jeshi la Libya Jumatano usiku wiki hii lilitangaza kuwa vikosi vyake hivi sasa vinaudhibiti kikamilifu mji wa Benghazi baada ya mapigano ya umwagaji damu.
Itakumbukwa kuwa, mji wa Benghazi ulikumbwa na mapigano makali kati ya vikosi vya jeshi la serikali na wanamgambo wa Baraza la Mapinduzi ya Benghazi ambao wana uhusiano wa karibu na kundi la kigaidi la Daesh tangu miaka iliyopita. Nchi hiyo ilitumbukia katika dimbwi la ghasia za kisiasa na ukosefu wa amani mara baada ya kupinduliwa dikteta wa zamani wa nchi hiyo Kanali Muammar Gaddafi.
Libya pia hivi sasa ina serikali mbili moja ikiwa na makao yake mashariki na nyingine magharibi mwa nchi. Serikali yenye makao yake huko Tripoli inatambuliwa kama serikali ya umoja wa kitaifa na ilishika hatamu za uongozi nchini humo mwezi Machi mwaka jana kwa upatanishi wa Umoja wa Mataifa.