Jaji Mkuu Kenya amuonya Rais Uhuru, usivunje imani ya wananchi
Jaji Mkuu wa Kenya amemuonya Rais Uhuru Kenyatta wa nchi hiyo akimtaka kuacha kuvunja imani ya wananchi kwa mahakama za nchi hiyo.
Jaji Mkuu wa Kenya, David Maraga amesema hayo baada ya Rais wa nchi hiyo kusema kuwa, mrengo wa upinzani unataka kutumia vyombo vya mahakama kwa ajili ya kushinda uchaguzi mkuu ujao. Kenyatta amesema serikali yake haitaruhusu wapinzani wake kutumia mahakama kwa ajili ya kuitishia Kamisheni Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) wakidhani kwamba, watashinda uchaguzi wa Rais kupitia mlango wa nyuma.
Jaji David Maraga amesema inatia wasiwasi kuona viongozi wa kisiasa wakikashifu vyombo vya mahakama kutokana na uelewa usio sahihi, suala ambalo amesisitiza kuwa, linaweza kuvunja imani ya wananchi kwa taasisi hiyo.
Jaji Mkuu wa Kenya amemtahadahrisha Rais Uhuru Kenyatta asivunje imani ya raia kwa mahakama za nchi hiyo.
Matamshi hayo yanahesabiwa kuwa malumbano makali zaidi baina ya vinara wa mihimuli hiyo miwili mikuu ya dola nchini Kenya wiki chache tu kabla ya uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika tarehe 9 Agosti.