Watu 14 wauawa 30 wajeruhiwa kaskazini mwa Cameroon
Watu 44 wameuawa na kujeruhiwa katika miripuko ya mabomu iliyotokea kaskazini mwa Cameroon.
Duru za usalama za Cameroon zimetangaza leo kuwa, watu 14 wameuawa katika miripuko miwili iliyotoka kwenye mji wa Waza wa kaskazini mwa Cameroon, karibu na mpaka wa nchi hiyo na Nigeria na wengine 30 wamejeruhiwa.
Duru hizo zimeongeza kuwa, kuna uwezekano mkubwa waliofanya mashambulizi hayo ya kigaidi ni wanamgambo wa Boko Haram. Habari zinasema kuwa, hali ya baadhi ya majeruhi hao ni mbaya sana, hivyo kuna uwezekano idadi ya waliouawa katika miripuko hiyo miwili, wakaongezeka.
Ijapokuwa mashambulizi ya kwanza makubwa ya magaidi wa Boko Haram yalitokea nchini Cameroon mwezi Machi 2014, lakini mashambulio ya genge hilo la kitakfiri yalianza takriban mwaka 2011 katika kona ya kaskazini mwa nchi hiyo. Mazingira ya kona hiyo ya kaskazini mwa Cameroon yanafanana sana na yale ya kaskazini mashariki mwa Nigeria ambako kunatokea mashambulizi mengi ya magaidi hao tangu mwaka 2009.
Mwaka 2013, genge la kigaidi la Boko Haram liliteka raia na viongozi wa kidini wa Cameroon, na mwaka 2014 likatangaza kuanzisha mashambulizi yenye lengo la kuunda serikali yake nchini Cameroon.
Hata hivyo kundi hilo la kigaidi limeshindwa kufanikisha lengo lake hilo kutokana na kukabiliwa na mashambulizi ya muungano wa kijeshi wa nchi nne za Cameroon, Niger, Nigeria na Chad.