Uganda kutuma wanajeshi elfu mbili Somalia kukabiliana na al Shabab
Serikali ya Uganda imesema kuwa imetuma wanajeshi wake elfu mbili huko Somalia ili kuendesha mapambano dhidi ya wanamgambo wa al Shabab wenye makao yao nchini Somalia.
Jenerali David Muhoozi Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Uganda amesema kuwa wanajeshi waho wa Uganda wa kikosi cha 22 wanatarajia kujiunga na wenzao wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika na kikosi cha nne cha kudumisha amani cha Umoja wa Mataifa huko Somalia katika mapambano dhidi ya al Shabab.
Jenerali Muhoozi ameongeza kuwa baadhi ya wanajeshi wa Uganda wameelekea Somalia pamoja na wanajeshi hao elfu mbili, ambao wanawajumuisha pia wanajeshi wa nchi kavu.
Serikali ya Uganda mwezi Mei mwaka huu ilitangaza mpango wa kuzidisha mara mbili idadi ya vikosi vyake vya ulinzi katika kalibu ya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika ili kuendesha mapambano dhidi ya kundi la kigaidi la al Shabab. Kundi la al Shabab limekuwa likitekeleza mashambulizi katika nchi jirani ya Kenya katika kulipiza kisasi hatua ya Kenya ya kutuma wanajeshi wake huko Somalia.