Libya kuongeza uzalishaji wake wa mafuta
Viongozi wa Libya wametangaza kuwa nchi hiyo ina mpango wa kuongeza uzalishaji wake wa mafuta hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu na kufikia mapipa milioni moja na laki mbili na eldfu hamsini kwa siku.
Mustafa Sanallah Mkuu wa Shirika la Taifa la Mafuta la Libya amesema leo kuwa lengo la nchi hiyo ni kufikisha mapipa milioni moja na laki mbili na elfu hamsini kwa siku hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu na mapipa milioni moja na laki tano ifikapo mwakani. Uzalishaji wa mafuta nchini Libya hivi karibuni ulipindukia mapipa milioni moja kwa siku. Mustafa Sanallah amesema anataraji kwamba Libya itaongeza uzalishaji wake wa mafuta na kufikia mapipa milioni mbili na laki moja kwa siku katika miaka minne hadi mitano ijayo.
Libya ni nchi iliyo na akiba kubwa zaidi ya mafuta barani Afrika, hata hivyo visima vingi vya mafuta nchini humo vilisimamisha uchimbaji au kudhibitiwa na magaidi baada ya kupinduliwa madarakani dikteta wa nchi hiyo Kanali Muammar Gaddafi mwaka 2011 na kujiri vita vya ndani nchini humo.