Harakati ya Kiislamu Nigeria yatahadharisha kuhusu uwezekano wa kuuawa Sheikh Zakzaky
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i32006-harakati_ya_kiislamu_nigeria_yatahadharisha_kuhusu_uwezekano_wa_kuuawa_sheikh_zakzaky
Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria imeitahadharisha serikali ya nchi hiyo kuhusu njama ya aina yoyote ya kutaka kumuua kiongozi wa harakati hiyo Sheikh Ibrahim Zakzaky anayeshikiliwa na vyombo vya usalama.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 20, 2017 00:21 UTC
  • Harakati ya Kiislamu Nigeria yatahadharisha kuhusu uwezekano wa kuuawa Sheikh Zakzaky

Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria imeitahadharisha serikali ya nchi hiyo kuhusu njama ya aina yoyote ya kutaka kumuua kiongozi wa harakati hiyo Sheikh Ibrahim Zakzaky anayeshikiliwa na vyombo vya usalama.

Taarifa iliyotolewa jana na Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imefichua kwamba, serikali ya nchi hiyo inafanya njama ya kutaka kumuua Sheikh Ibrahim Zakzaky na kuwashambulia wanachama wengine wa harakati hiyo.

Taarifa hiyo imeashiria kitendo cha kuwekwa wanajeshi katika maeneo ya kistratijia na yenye idadi kubwa ya watu kwenye miji mikubwa ya nchi hiyo na kusema kuwa: Wanajeshi hao wanasubiri amri ya kuanza kumwaga damu za raia wasio na hatia.

Taarifa ya Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imeitaka jamii ya kimataifa kuingilia kati kwa ajili ya kuzuia mauaji ya watu wasio na hatia nchini humo. 

Waislamu Nigeria wanataka kuachiwa huru Sheikh Zakzaky

Taarifa hiyo imesisitiza kuwa, kuuawa kwa Sheikh Ibrahim Zakzaky na wanachama wa harakati hiyo hakutakuwa na taathira yoyote kwa hali ya Nigeria na ameitaka serikali ya Abuja kukomesha mauaji ya halaiki dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo hususan wafuasi wa madhehebu ya Shia na kumwachia huru Sheikh Zakzaky.

Wimbi la mauaji ya Waislamu nchini Nigeria lilianza tarehe 13 Disemba mwaka 2015 baada ya jeshi la nchi hiyo kushambulia kituo cha kidini cha Waislamu wa madhehebu ya Shia katika mji wa Zaria na kuua mamia ya wafuasi wa Sheikh Ibrahim Zakzaky wakiwemo watoto wake watatu.