Watunisia waandamana kupinga maonyesho ya vichekesho ya Mzayuni nchini kwao
Watunisia wamefanya maandamano mjini Tunis kupinga maonyesho ya vichekesho ya Michel Boujenah Mzayuni mwenye uraia wa nchi mbili za Ufaransa na Tunisia nchini mwao.
Katika maandamano hayo raia wa nchi hiyo waliokuwa na mabango yenye jumbe za kupinga jinai za Israel na bendera za taifa la Palestina, wameitaka serikali ya Tunis kufunga mara moja maonyesho ya Mzayuni huyo ndani ya nchi yao.
Waandamanaji wamekusanyika mbele ya mahkama moja ya mjini Tunis na kulaani mahusiano yaliyopo kati ya nchi yao na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel. Kadhalika Watunisia wamelaani vikali kitendo cha nchi yao cha kutekeleza siasa za Israel kupitia mashinikizo ya utawala haramu wa Kizayuni. Inafaa kuashiria kuwa, Michel Boujenah Mzayuni na msanii wa vichekesho anayeishi Ufaransa ni maarufu sana kwa uungaji mkono wake kwa Mayahudi na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel unaozikalia kimabavu ardhi za Palestina.
Ni mara kadhaa ambapo raia wa Tunisia wamekuwa wakifanya maandamano kuwaunga mkono raia madhlum wa Palestina na kuitaka serikali ya nchi hiyo kukata mahusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel.