Amnesty International :Ubakaji dhidi ya raia umekithiri Sudan Kusini
Jumuiya ya kutetea haki za binadamu ya Amnesty International imetahadharisha kuhusu ongezeko kubwa la ukatili wa kingono na ubakaji wa maelfu ya wanawake, wasichana na hata wanaume katika nchi za Sudan Kusini.
Ripoti ya Amnesty International imetahadharisha kuhusu vitendo hivyo viovu vya kubakwa na kunajisiwa maelfu ya raia Sudan Kusini tangu baada ya kuanza vita na mivutano ya kisiasa na kikabila nchini humo baina ya wafuasi wa Rais Salva Kiir na makamu wake wa zamani, Rieck Machar na imelaani tabia ya kuwapa kinga na kuwakingia kifua watu wanaofanya uhalifu na ukatili huo.
Ripoti ya Amnesty International imeashiria hali mbaya ya kinafsi ya wahanga wa vitendo hivyo viovu na kueleza wasiwasi wake kuhusu ongezeko la uhalifu wa kuwabaka na kuwanajisi raia unaofanyika kwa mpangilio maalumu.
Katika miezi michache ya hivi karibuni kumeripotiwa kesi 170 za vitendo vya ubakaji nchini Sudan Kusini na 20 miongoni mwa waliofanyiwa ukatili huo ni wanaume.
Sudan Kusini ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2013 miaka miwili tu baada ya kujitenga na Sudan. Maelfi ya watu wameuawa na mamilioni ya wengine wamelazimika kuwa wakimbizi kutokana na mapigano hayo.