Jul 28, 2017 04:05 UTC
  • Zaidi ya watu 40 wauawa katika shambulio la Boko Haram nchini Nigeria

Zaidi ya watu 40 wameuawa nchini Nigeria na makumi ya wengine kujeruhiwa kufuatia shambulio la kundi la kigaidi la Boko Haram kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Duru za usalama za Nigeria zimethibitisha kutokea mauaji hayo na kueleza kuwa, zaidi ya watu 40 wameuawa katika shambulio la Boko Haram dhidi ya timu ya wafanyakazi wa kampuni ya taifa ya kuchimba mafuta nchini humo.

Kwa mujibu wa duru za kieneo, mauaji hayo ni makubwa kabisa kuwahi kufanya na wanagmabo wa Boko Haram katika siku za hivi karibuni. Siku ya Jumatano pia, wahandisi 10 wa Shirika la Taifa la Mafuta la Nigeria walitekwa nyara na wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram na kupelekwa kusikojulikana.

Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria ambaye serikali yake inakosolewa kwa kushindwa kukabiliana na Boko Haram

Aidha Jumanne iliyopita, viwiliwili vinane vya wanajeshi na cha raia mmoja vilipatikana kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Tangu lilipoanzisha mashambulizi yake nchini Nigeria mwaka 2009 hadi hivi sasa, genge hilo limeshaua watu wasiopungua 20 elfu na kuwafanya wakimbizi zaidi ya watu milioni mbili na laki sita.  

Serikali ya Rais Muhamadu Buhari inakosolewa vikali kwa kushindwa kukabiliana na kundi la Boko Haram. Hata kikosi cha pamoja cha nchi za eneo kilichoundwa kwa shabaha ya kukabiliana na wanamgambo hao wa Boko Haram kinaonekana kushindwa kufikia malengo yake. 

 

 

 

Tags