Wawili waliuawa katika shambulio nyumbani kwa Makamu wa Rais wa Kenya
Watu wawili waliuawa juzi katika shambulio lililofanywa katika makazi ya Makamu wa Rais wa Kenya, William Rutto. Hayo yameelezwa na polisi siku kadhaa kabla ya nchi hiyo ya Kiafrika kuendesha uchaguzi wa Rais tarehe nane Agosti.
Imebainika kuwa, mvamizi aliyekuwa na silaha na polisi mmoja waliuliwa juzi usiku baada ya polisi kufyatuliana risasi na mvamizi huyo nje ya makazi ya William Ruto katika mji wa magharibi wa Eldoret. Mlinzi mmoja pia alijeruhiwa katika shambulio hilo.
Polisi imeongeza kuwa, Makamu wa Rais wa Kenya William Ruto ambaye ni mgombea mwenza wa Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi ujao na familia yake hakuwepo nyumbani wakati huo.
Wakati huo huo Wanyama Musiambo ambaye ni Mratibu wa Mkoa wa Rift Valley amesema kuwa, ilidhaniwa kuwa watu wawili ndio waliofanya uvamizi huo kwa kuzingatia milio ya risasi iliyokuwa ikisikika. Hata hivyo amesema baada ya kumdhiti mvamizi ndipo ilipobainika kuwa mtu mmoja ameuawa pamoja na afisa mmoja wa polisi aliyeuawa na mvamizi huyo.
Uchunguzi mwingine unaonyesha kuwa, awali mvamizi hakuwa na silaha lakini aliingia katika ghala la silaha la polisi na kutumia silaha hizo.