Askari 12 wa Uganda wauawa nchini Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i32522-askari_12_wa_uganda_wauawa_nchini_somalia
Jeshi la Uganda limetangaza kuwa, askari 12 wa nchi hiyo wameuawa katika shambulizi lililofanywa na wapiganaji wa kundi la kigaidi la al Shabab kusini mwa Somalia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 31, 2017 11:05 UTC
  • Askari 12 wa Uganda wauawa nchini Somalia

Jeshi la Uganda limetangaza kuwa, askari 12 wa nchi hiyo wameuawa katika shambulizi lililofanywa na wapiganaji wa kundi la kigaidi la al Shabab kusini mwa Somalia.

Taarifa iliyotolewa leo na jeshi la Uganda (UPDF) imesema kuwa, askari hao 12 waliuawa jana katika shambulizi la kuvizia lililofanywa na wapiganaji wa al Shabab katika eneo la  Lower Shebelle huko kusini mwa Somalia.

Taarifa hiyo imesema askari hao walikuwa sehemu ya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika (AMISOM) nchini Somalia. Imeongeza kuwa askari wengine 7 wamejeruhiwa. 

Mapema jana Naibu Gavana wa Mkoa wa Lower Shabelle, Ali Nur alisema kuwa askari 23 wa kikosi cha AMISOM na mmoja wa jeshi la Somalia wameuwa katika shambulizi la kuvizia la al Shabab.

Mauaji hayo ya askari 12 wa Uganda yamefanyika wiki mbili tu baada ya Kampala kutangaza kwamba, itatuma wanajeshi 2000 nchini Somalia kwa ajili ya kupambana na wapiganaji wa kundi la al Shabab. 

Jeshi la Uganda nchini Somalia

Jenerali David Muhoozi, Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Uganda amesema kuwa wanajeshi hao wanatarajia kujiunga na wenzao wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika na wale wa Umoja wa Mataifa huko Somalia katika mapambano dhidi ya al Shabab.

Kundi la al Shabab ambalo limefukuzwa katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu limekuwa likifanya mashambulizi ya kujilipua kwa mabomu ndami ya ardhi ya Somalia na katika nchi jirani kama Kenya.