UN yaunga mkono kurejeshwa amani nchini Sudan Kusini
Umoja wa Mataifa umekaribisha kurejeshwa amani na kuhitimishwa mivutano nchini Sudan Kusini.
Jean-Pierre Lacroix, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Haki za Binaadamu alikutana Jumatano ya jana na Rais Salva Kiir Mayardit wa Sudan Kusini na kusisitizia udharura wa kuwepo mashirikiano zaidi baina ya viongozi wa nchi hiyo changa barani Afrika kwa ajili ya kuhitimisha machafuko na vitendo vya utumiaji mabavu.
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Haki za Binaadamu na Rais wa Sudan Kusini vilevile wamebadilishana mawazo kuhusu mwenendo wa amani, ubunifu wa Jumuiya ya Ushirikiano na Maendeleo ya Pembe ya Afrika-IGAD kwa ajili ya kuhuisha makubaliano ya kisiasa, mazungumzo ya kitaifa, kutumwa askari wa kieneo kwa ajili ya kusimamia amani na hali ya kibinaadamu inayotawala nchini humo kwa sasa. Sudan Kusini iliyojitangazia uhuru mwaka 2011, ilitumbukia katika hali ya mchafukoge na vita vya ndani tangu mwezi Disemba mwaka 2013, ambavyo hadi sasa vimesababisha makumi ya maelfu ya watu kuuawa na wengine zaidi ya milioni tatu kuwa wakimbizi. Vita hivyo vinawajumuisha askari wa serikali ya Rais Salva Kiir na wale watiifu kwa makamu wa zamani wa rais, Riek Machar.