Italia: Vitisho vya Khalifa Haftar havitazuia operesheni zetu katika Bahari ya Mediterania
Balozi wa Italia nchini Libya, Giuseppe Perrone amesema kuwa vitisho vilivyotolewa na kamanda wa Jeshi la Taifa la nchi hiyo Khalifa Haftar, havitazuia majukumu ya Italia katika maji ya eneo hilo.
Perrone amesema, vitisho vya Haftar kwamba jeshi la Libya litazishambulia meli za kijeshi za Italia katika maji ya nchi hiyo haviwezi kuzuia utekelezaji wa majukumu ya jeshi la Italia na kutuma meli zake za kijeshi katika maji ya taifa hilo kwa lengo la kuzuia misafara ya wafanyamagendo ya binaadamu wanaowasafirisha wahajiri haramu kwenda barani Ulaya.
Balozi wa Italia nchini Libya ameongeza kuwa, majukumu ya jeshi la nchi yake yalipitishwa wiki iliyopita na ujumbe wa serikali ya Rome kwa kushirikiana na viongozi wa Libya wakiongozwa na Fayez al-Sarraj, Waziri Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya.
Bunge la Italia lilikubali pendekezo la al-Sarraj la kutumwa meli za kivita katika maji ya Libya ili kukabiliana na wimbi la wahajiri haramu. Hata hivyo kamanda wa Jeshi la Taifa la nchi hiyo, Khalifa Haftar ametoa amri ya kukabiliana na meli hizo katika maji ya ya Libya kutishia kuzishambulia meli hizo.