Umoja wa Mataifa wagundua makaburi ya umati kaskazini mwa Mali
Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Mali (MINUSMA) kimegundua makaburi ya umati kaskazini mwa nchi hiyo ya Kiafrika.
Taarifa ya MINUSMA imesema makaburi hayo yamegunduliwa katika kijiji cha Anefis, yapata kilomita 100 kusini magharibi mwa mji wa Kidal, kaskazini mwa nchi.
MINUSMA imesema kwa sasa haijaweza kubaini sababu za kuuawa, idadi na utambulisho wa maiti zilizopatikana katika makaburi hayo ya umati.
Eneo la kaskazini mwa Mali limekuwa uwanja wa makabiliano kati ya magenge ya wapiganaji wa Tuareg kwa upande mmoja na makundi yenye misimamo ya kufurutu ada na maafisa usalama kwa upande mwingine.
Mwezi uliopita, duru za usalama za Mali zilitangaza habari ya kupatikana miili ya wanajeshi wanane wa serikali, kaskazini mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika, waliouawa katika shambulio la watu wenye silaha katika maeneo ya Gao na Menaka.
Mwezi Machi 2012, maeneo ya kaskazini mwa Mali yalitekwa na makundi yenye misimamo mikali ambayo yana uhusiano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaida; na mwaka mmoja baadaye, kikosi cha MINUSMA kilitumwa nchini humo kwa ajili ya kupambana na magenge hayo ya kitakfiri.