Aug 08, 2017 07:49 UTC
  • Boko Haram yaua wavuvi 31 kaskazini mwa Nigeria

Kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram limeua makumi ya wavuvi baada ya kuvamia visiwa viwili vya eneo la Ziwa Chad, kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Shirika la habari la AFP limeripoti kuwa, magaidi hao wa kitakfiri walivamia visiwa vya Duguri na Dabar Wanzam kwenye kingo za Ziwa Chad, na kuua wavuvi 31 kwa kuwamiminia risasi na wengine kwa kuwanyonga, kuwadunga visu au kuwagonga kwa kifaa butu.

Mauaji hayo yamefanyika wiki moja baada ya maafisa wa majeshi ya Nigeria, Niger, Cameroon na Chad kuondoa marufuku ya kufanya uvuvi katika Ziwa Chad ambalo maji yake yapo katika mipaka ya nchi hizo nne za magharibi mwa Afrika.

Wanachama wa Boko Haram

Jeshi na Nigeria na maafisa wa serikali ya nchi hiyo hawajatoa tamko lolote kuhusu hujuma hiyo ya Jumamosi, ambayo wakaazi wa visiwa hivyo wanasema wavuvi 14 wameuawa katika eneo la Duguri na 17 katika eneo la Dabar Wanzam.

Hii ni katika hali ambayo, watu 12 waliuawa kusini mashariki mwa Nigeria na makumi ya wengine kujeruhiwa baada ya watu waliokuwa na silaha kuvamia kanisa moja na kuanza kuwamiminia watu risasi Jumapili iliyopita. Inasadikiwa kuwa, huenda waliotekeleza shambulio hilo ni wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram.

Tangu lilipoanzisha mashambulizi yake nchini Nigeria mwaka 2009 hadi hivi sasa, genge hilo limeshaua watu wasiopungua 20 elfu na kuwafanya wakimbizi zaidi ya watu milioni mbili na laki sita.  

Tags