Wakenya watakiwa kudumisha amani; waangalizi wataka madai ya upinzani kuchunguzwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i32962-wakenya_watakiwa_kudumisha_amani_waangalizi_wataka_madai_ya_upinzani_kuchunguzwa
Waangalizi wa kimataifa wa uchaguzi wa Kenya uliofanyika siku ya Jumanne wametoa wito na kuwataka wananchi wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki kudumisha amani na utulivu.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Aug 10, 2017 10:09 UTC
  • Wakenya watakiwa kudumisha amani; waangalizi wataka madai ya upinzani kuchunguzwa

Waangalizi wa kimataifa wa uchaguzi wa Kenya uliofanyika siku ya Jumanne wametoa wito na kuwataka wananchi wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki kudumisha amani na utulivu.

Wito huo umetolewa katika hali ambayo, Wakenya wangali wanasubiri matokeo rasmi ya mwisho ya uchaguzi huo huku hali ya wasiwasi ikitanda baada ya watu watano kuuawa katika ghasia na machafuko yaliyozuka katika baadhi ya miji ya nchi hiyo. 

Wasimamizi hao wa kimataifa wapatao 400 kutoka Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, Umoja wa Afrika na asasi nyingine za kiraia wamesema kuwa, Wakenya wanapaswa kuwa watulivu katika kipindi hiki cha kusubiri matokeo ya mwisho na kujiepusha na vitendo vya uhatarishaji amani.

Wakati huo huo, waangalizi wa uchaguzi huo wa Kenya wamesema kuwa, wanataka madai ya Muungano wa upinzani NASA kuwa mfumo wa Tume ya Uchaguzi na Mipaka IEBC ulidukuliwa na matokeo kubadilishwa, yafanyiwe uchungizi wa kina.

Waangalizi wa Umoja wa Ulaya katika uchaguzi wa Kenya

Kiongozi wa waangalizi wa Umoja wa Ulaya Marietje Schaake amesema kuwa, ni muhimu sana kushughulikia madai hayo ili kuweka kila kitu wazi kuhusu uchaguzi huo.

Wito kama huu umetolewa pia na waangalizi kutoka Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Madola na wale kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kuhusu kuuawa kwa watu watano katika mtaa wa Mathare jijini Nairobi siku ya Jumatano, na katika maandamano ya mjini Kisumu, waangalizi wa uchaguzi huo wametaka maafisa wa polisi kuacha kutumia nguvu kupita kiasi.