Uchaguzi Kenya: Kofi Annan amtaka Raila Odinga atumie njia za kisheria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i33106-uchaguzi_kenya_kofi_annan_amtaka_raila_odinga_atumie_njia_za_kisheria
Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan, ambaye alikuwa mpatanishi mkuu baada ya mzozo wa kisiasa nchini Kenya miaka kumi iliyopita, ametoa wito kwa walioshindwa katika uchaguzi wa Kenya kutumia mifumo ya kisheria kwa ajili ya kutafuta haki.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 13, 2017 23:04 UTC
  • Uchaguzi Kenya: Kofi Annan amtaka Raila Odinga atumie njia za kisheria

Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan, ambaye alikuwa mpatanishi mkuu baada ya mzozo wa kisiasa nchini Kenya miaka kumi iliyopita, ametoa wito kwa walioshindwa katika uchaguzi wa Kenya kutumia mifumo ya kisheria kwa ajili ya kutafuta haki.

Katibu Mkuu huyo wa zamani wa UN amempongeza Uhuru Kenyatta kwa ushindi wake na pia akamsifu Raila Odinga kwa kuendesha kampeni zake kwa njia ya amani.

"Namshukuru kiongozi wa upinzani Raila Odinga kwa kampeni za uchaguzi za amani alizoiendesha. Amekuwa mtetezi jasiri wa demokrasia," amesema Dkt Annan kupitia taarifa yake.

Aidha Kofi Annan amaesema pia kama ninavyomnukuu: 

"Ninamhimiza Bwana Raila Odinga  afuatilie malalamiko yake kupitia mifumo ya kisheria iliyowekwa na aweke maslahi ya taifa mbele, kama alivyofanya kwa uzalendo mara nyingi.

Raila Odinga aliyegombea kiti cha urais Kenya kwa tiketi ya chama cha ODM

Hayo yanajiri huku, kinara wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga akiwataka wafuasi wake wasiende kazini leo Jumatatu na wajiandae kupokea kile alichokitaja kuwa maelekezo na tangazo zito litakalotikisa taifa siku ya Jumanne.

Kwa mujibu wa Kamisheni ya Taifa ya Kutetea Haki za Binadamu, watu 24 wameuawa kwa kufyatuliwa risasi hadi sasa, katika maandamano na ghasia za kupinga ushindi wa Rais Kenyatta.

Matokeo rasmi ya IEBC yanaonyesha kuwa, Uhuru Kenyatta aliyegombea kwa tiketi ya chama cha Jubilee alipata ushindi baada ya kujizolea kura 8,203,290 sawa na asilimia 54.27 ya kura zote, huku mshindani wake mkuu Raila Odinga  aliyegombea kwa tiketi ya ODM akipata kura 6,762,224 sawa na asilimia 44.74 ya kura zote.