Mrithi mtarajiwa wa rais wa Zimbabwe alazwa hospitalini nchini Afrika Kusini
Makamu wa Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa mmoja wa wanasiasa wanaotarajiwa kumrithi Rais wa nchi hiyo Robert Mugabe amesafrishwa kupelekwa nchini Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu.
Rais Mugabe mwenye umri wa miaka 94 ametoa tangazo hilo leo baada ya Mnangagwa kushindwa kuhudhuria sherehe za kuadhimisha Siku ya Mashujaa zilizofanyika Harare mji mkuu wa nchi hiyo.
"Bado hajarejea kutoka hospitalini Johannesburg", alisema Mugabe katika hotuba aliyotoa katika eneo la Ekari ya Mashujaa wa taifa. Hata hivyo hakutoa ufafanuzi zaidi.
Emmerson Mnangagwa na Pelekezela Mphoko ni mamakamu wa Rais wa Robert Mugabe serikalini na ndani ya chama tawala cha Zanu-PF, lakini Mnangagwa ndiye anayeelekea zaidi kuwa mrithi wa Mugabe tangu alipoteuliwa kushika wadhifa wa umakamu wa rais mwaka 2014.
Suala la nani atamrithi Mugabe limezusha mpasuko na mgawanyiko mkubwa ndani ya chama tawala nchini Zimbabwe kukiwepo mirengo miwili, mmoja unaomuunga mkono Mnangagwa na mwengine wa mke wa Mugabe, Grace.
Vyombo vya habari vya ndani vimetangaza kuwa Emmerson Mnangagwa amedhurika kwa kula chakula kilichoharibika.
Mnangagwa, ambaye anajulikana kwa lakabu ya Mamba katika lugha ya Kishona aliteuliwa kuwa makamu wa rais baada ya Mugabe kumtimua Bi Joice Majuru aliyekuwa akishikilia cheo hicho kwa muda wa miaka 10.
Bi Majuru ameunda chama chake cha siasa ambacho ni sehemu ya mrengo wa upinzani unaotazamiwa kuchuana na Rais Mugabe katika uchaguzi wa rais utakaofanyika mwaka ujao wa 2018.../