Kiongozi wa upinzani wa Zambia aachiwa huru, afutiwa kesi ya uhaini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i33224-kiongozi_wa_upinzani_wa_zambia_aachiwa_huru_afutiwa_kesi_ya_uhaini
Kinara wa upinzani nchini Zambia, Hakainde Hichilema ameachiwa huru na kutoka gerezani hii leo baada ya Mkuu wa Mashtaka ya Umma kumfutia mashtaka ya uhaini.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 16, 2017 09:51 UTC
  • Kiongozi wa upinzani wa Zambia aachiwa huru, afutiwa kesi ya uhaini

Kinara wa upinzani nchini Zambia, Hakainde Hichilema ameachiwa huru na kutoka gerezani hii leo baada ya Mkuu wa Mashtaka ya Umma kumfutia mashtaka ya uhaini.

Jaji wa Mahakama Kuu mjini Lusaka, Charles Chanda amemuambia Hichilema na mpambe wake waliokuwa wakiandamwa na tuhuma za uhaini kuwa: "Kwa sasa mpo huru kwenda nyumbani baada ya Mkuu wa Mashtaka ya Umma kuondoa mashtaka ya jaribio la mapinduzi dhidi yenu. Hata hivyo mfahamu kuwa hampo huru kikamilifu, mnaweza kupandishwa kizimbani tena kwa kesi hii."

Chama cha upinzani cha United Party for National Development (UPND) kimethibitisha habari hizo katika ukurasa rasmi wa mtandao wa kijamii wa Twitter na kusema kuwa kiongozi wao ameachiwa huru leo, siku ambayo kesi dhidi yake ilitazamiwa kuanza.

Hakainde Hichilema

Siku chache zilizopita, duru za habari ziliarifu kuwa, Hichilema ataachiwa huru kufuatia makubaliano yaliyofikiwa kati ya serikali, vyombo vya mahakama na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola.

Hichilema ambaye ni mkuu wa chama cha UPND alikamatwa na vyombo vya usalama mapema mwezi Aprili mwaka huu, kwa tuhuma za kupanga njama ya kuipindua serikali. 

Vyombo vya usalama vilidai kuwa vimemtia nguvuni mwanasiasa huyo wa upinzani kwa kuzuia msafara wa magari ya Rais Edgar Lungu wa nchi hiyo ya Kiafrika, magharibi mwa nchi. 

Serikali ya Zambia imekuwa ikikosolewa kwa kuwawekea mbinyo viongozi wa upinzani na wakosoaji wake.