Uganda yafungua kambi mpya kwa ajili ya wakimbizi wa Sudan Kusini
Uganda imefungua kambi mpya kwa ajili ya kuwapokea maelfu ya wakimbizi wa Sudan Kusini wanaozidi kumiminika kila uchao katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Kanali ya televisheni ya Press TV imeripoti kuwa, kambi hiyo imefunguliwa katika wilaya ya Arua, kaskazini mwa Uganda na inatazamiwa kuwapa hifadhi wakimbizi wapatao 40,000 watakaoingia nchini humo katika kipindi cha wiki chache zijazo.
Hivi karibuni, Mratibu wa Umoja wa Mataifa nchini Uganda, Rosa Malango alisema kuwa, wakimbizi elfu mbili wa Sudan Kusini huingia kila siku katika nchi ya Uganda na inatarajiwa kuwa, hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu wa 2017 jumla ya wakimbizi laki nne kutoka Sudan Kusini watakuwa wameingia katika nchi hiyo.
Haya yanajiri katika hali ambayo, mwezi Februari mwaka huu, Umoja wa Mataifa ulisema wakimbizi 52,000 raia wa Sudan Kusini waliingia nchini Uganda mwezi wa Januari pekee, kutokana na kuendelea kushuhudiwa mauaji na machafuko katika nchi yao na kubainisha kuwa, watu wanauawa kwa umati na kutendewa jinai nyinginezo za kutisha katika eneo la Kajo-Keji.
Mapigano ya ndani nchini Sudan Kusini yalianza mwaka 2013 kati ya jeshi linalomuunga mkono Rais Salva Kiir na wanamgambo watiifu kwa aliyekuwa makamu wa rais wa nchi hiyo Riek Machar. Wakati huo Rais Salva Kiir alimtuhumu makamu wake kuwa alifanya jaribio la kuipindua serikali yake.
Maelfu ya watu wameuawa na wengine zaidi ya milioni moja wamelazimika kuwa wakimbizi kutokana na mapigano hayo.