Sudan Kusini yakabiliwa na uhaba wa mafuta ya petroli
Vituo vya mafuta ya petroli Sudan Kusini vinakabiliwa na uhaba mkubwa wa bidhaa hiyo pamoja na kuwa nchi hiyo ina utajiri wa mafuta ghafi ya petroli.
Nchi hiyo ya mashariki mwa Afrika imeshindwa kuagiza mafuta yaliyosafishwa nje ya nchi kutokana na mapigano yanayoendelea nchini humo na hivyo kuhatarisha usafirishaji mafuta.
Aidha wafanyabiashara wanaoagiza mafuta kutoka nje ya nchi wameshindwa kufanya hivyo kutokana na mfumuko wa bei ambao sasa umefika asilimia 800.
Katika miezi ya hivi karibuni usafiri wa mabasi na pikipiki maarufu kama boda boda umesitishwa katika mji mkuu Juba kutokana na uhaba wa mafuta. Hivi sasa biashara kote Sudan Kusini zimevurugika kutokana na wafanyabiashara kushindwa kusafirisha bidhaa zao.
Vita vya ndani nchini humo vilivyoanza Disemba 2013 vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. Nchi hiyo ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kuipindua serikali yake. Jitihada za kieneo na kimataifa za kuutatua mgogoro huo hazijazaa matunda.