Ongezeko la asilimia 58 la bidhaa za Iran zinazouzwa Kenya
Kumekuwa na ongezeko la asilimia 58 ya bidhaa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zinazouzwa nchini Kenya katika kipindi cha miezi minne iliyopita ikilinganishwa na muda kama huo mwaka 2016.
Farzad Piltan Mkurugenzi wa Idara ya nchi za Kiafrika na Kiarabu katika Shirika la Ustawi wa Biashara la Iran amesema: "Bidhaa za Iran zilizouzwa Kenya katika miezi minne iliyopita zimefika thamani ya dola milioni 32 katika hali ambayo muda sawa na huu mwaka 2016 kiwango hicho kilikuwa cha dola milioni 20.
Piltan amesema aghalabu ya bidhaa za Iran zinazouzwa Kenya ni pamoja na vyakula, seruji au simiti na petrokemikali.
Mwezi Mei Kenya ilitangazwa kuwa inaongoza katika ununuzi wa bidhaa kutoka Iran barani Afrika na ni ya 15 kwa ujumla katika ununuzi wa bidhaa za Iran duniani.
Kwa mujibu wa Murtadha Daylan, mwambata wa kibiashara wa Iran mjini Nairobi, "Kenya ni nchi ya 15 inayonunua kwa wingi bidhaa kutoka Iran kwa mujibu wa takwimu za mwezi Machi mwaka 2017."
Afisa huyo wa masuala ya kibiashara katika ubalozi wa Iran nchini Kenya amesema kati ya mipango ya baadaye ni kuundwa chumba cha kibiashara cha pamoja baina ya Iran na Kenya kwa ajili ya kubadilishana habari na kupunguza matatizo ya kibiashara baina ya pande mbili.