Maficho kadhaa ya magaidi yasambaratishwa nchini Algeria
Wizara ya Ulinzi ya Algeria imetangaza habari ya kuangamizwa maficho kadhaa ya magaidi kaskazini mwa nchi hiyo.
Katika taarifa yake ya jana Jumamosi, Wizara ya Ulinzi ya Algeria imesema, maficho manne ya magaidi yamesambaratishwa katika operesheni mbili tofauti zilizofanywa na jeshi la nchi hiyo kwenye mikoa miwili ya Tizi Ouzou na Tipaza, ya kaskazini mwa Algeria.
Taarifa ya jeshi hilo imeongeza kuwa, jeshi la Algeria limefanikiwa kukamata silaha nyingi za magaidi hao.
Aidha imesema, kikosi maalumu cha kupambana na uhalifu wa kimataifa kimefanya operesheni kadhaa maalumu katika maeneo ya kusini mwa Algeria na kufanikiwa kuwatia mbaroni wafanya magendo 19 na kukamata vifaa maalumu vya kutafutia dhahabu ardhini vilivyokuwa vinatumiwa na wahalifu hao.
Algeria inakabiliwa na hali tete ya kiusalama kutokana na machafuko yanayoendelea katika baadhi ya nchi zinazopakana nayo kama vile Libya na Mali. Makundi mbalimbali ya kigaidi na ya magendo ya mihadarati yanajipoenyeza mara kwa mara katika ardhi ya Algeria.
Kwa upande wao viongozi wa Algeria wamekuwa wakisisitizia mara kwa mara ulazima wa vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo kuwa macho muda wote katika kukabiliana na mashambulizi na vitisho vya kiusalama vinavyoweza kusababishwa na magenge yenye misimamo ya kuchupa mipaka.