Waislamu Nigeria waitaka Marekani kusitisha uuzaji silaha kwa serikali ya Abuja
Waislamu wa Nigeria wameitumia barua serikali ya Marekani wakiitaka isitishe kuiuzia silaha na zana za kijeshi serikali ya Nigeria.
Katika barua hiyo iliyotumwa kwa serikali ya Marekani, Abdul Rahman Abu Bakr, mwenyekiti wa kamati ya kumkomboa kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria Sheikh Ibrahim Zakzaky ameashiria ukandamizaji wa haki za binadamu unaofanywa na serikali ya Nigeria na kusema: Washington inapaswa kusitisha uuzaji wa zana za kijeshi kwa serikali ya Abuja.
Barua hiyo imesisitiza kuwa, iwapo Marekani itaendelea kuiuzia silaha serikali ya Nigeria basi itakuwa mshirika katika uhalifu na jinai zinazofanywa na serikali ya Abuja.
Vilevile Waislamu wa Nigeria wametoa wito wa kuwekewa vikwazo vya silaha serikali ya nchi hiyo na kuwazuia viongozi wa Abuja kufanya safari za kimataifa.
Mwezi Disemba mwaka 2015 jeshi la serikali ya Nigeria lilishambulia kituo cha kidini cha Waislamu wa madhehebu ya Shia katika mji wa Zaria na kuua mamia miongoni mwao. Jeshi la Nigeria pia lilimkamata kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo, Sheikh Ibrahim Zakzaky na kumpeleka kusikojulikana.