Watu 25 wauawa katika mapigano eneo lenye utajiri wa mafuta Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i34565-watu_25_wauawa_katika_mapigano_eneo_lenye_utajiri_wa_mafuta_sudan_kusini
Waasi wa Sudan Kusini wameshambulia wanajeshi wa serikali katika jimbo la Unity ambalo lina visima vingi vya mafuta ambapo watu 25 wameuawa wakiwemo raia kadhaa.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Sep 19, 2017 11:01 UTC
  • Watu 25 wauawa katika mapigano eneo lenye utajiri wa mafuta Sudan Kusini

Waasi wa Sudan Kusini wameshambulia wanajeshi wa serikali katika jimbo la Unity ambalo lina visima vingi vya mafuta ambapo watu 25 wameuawa wakiwemo raia kadhaa.

Taarifa zinasema kati ya waliouawa katika mapigano hayo ya Jumatatu mjini NhialDiu ni wanawake, wazee na maafisa wa polisi.

Msemaji wa waasi Lam Paul Gabriel amesema ni watu 18 waliouawa katika mapigano hayo huku serikali ikisema imefanikiwa kuwarudisha nyuma waasi. Msemaji wa jeshi la Sudan Kusini, Dickson Gatluak Jock amesema shambulizi hilo limefanywa wakati wa kuanza mazungumzo mjini NhialDiu baina ya koo hasimu zinazounga mkono waasi na serikali kwa lengo la kurejesha amani katika eneo hilo.

Askari wa Jeshi la Sudan Kusini

Uchimbaji mafuta ulisitishwa katika jimbo la Unity baada ya kuibuka mapigano mapya Sudan Kusini Disemba mwaka 2013. Mapigano hayo yalianza baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kupindua serikali yake.

Vita hivyo vya ndani  vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi katika nchi hiyo iliyojitangazia uhuru mwaka 2011 baada ya kujitenga na Sudan.