Wanaochochea machafuko Sudan Kusini wawajibishwe
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i34645-wanaochochea_machafuko_sudan_kusini_wawajibishwe
Wito umetolewa kuhakikisha kwamba wanaochochea machafuko ya Sudan Kusini wanawajibishwa na pia misaada ya kibinadamu iwafikie wanaoihitajia katika nchi hiyo.
(last modified 2026-03-27T07:58:19+00:00 )
Sep 21, 2017 02:46 UTC
  • Wanaochochea machafuko Sudan Kusini wawajibishwe

Wito umetolewa kuhakikisha kwamba wanaochochea machafuko ya Sudan Kusini wanawajibishwa na pia misaada ya kibinadamu iwafikie wanaoihitajia katika nchi hiyo.

Wito huo umetolewa kwenye mkutano maalumu kuhusu hali ya kibinadamu na usaidizi Sudan Kusini ulioandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuratibu Misaada ya Kibinadamu OCHA na kushirikisha wadau mbalimbali wa kimataifa ukiwemo Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya, na mashirika ya kimataifa ya misaada.

Wadau hao wametoa dukuduku zao kuhusu hali inayoendelea Sudan Kusini. Akizungumza katika kikao hicho,  Bi Sessouma Minata Samate Kamishina wa Muungano wa Afrika amesisitiza kuwa kushughulikia hali ya kibinadamu na kuunga mkono mchakato wa amani katika nchi hiyo ni jukumu la jamii ya kimataifa.

Askari wa Jeshi la Sudan Kusini

Naye kamishina wa Umoja wa Ulaya wa misaada ya kibinadamu Christos Stylianides ameonya kuhusu wanaochochea machafuko Sudan Kusini na kusema, "Hatutonyamaza na tusikae kimya tukaliangalia taifa hili likisambaratika, waharibifu lazima waambiwe bayana kwamba watawajibishwa kwa vitendo vyao, tutaunga mkono juhudi za Umoja wa Mataifa za kuwawajibisha.

Sudan Kusini ilijitenga na Sudan mwaka 2011, na Disemba mwaka 2013 ikatumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kupindua serikali yake. Mapigano hayo yamepelekea makumi ya maelefu kuuawa na malaki ya wengine kukimbia makazi yao. Juhudi za kusaka amani nchini humo zimefeli hadi sasa.