Mchungaji apandishwa kizimbani kwa jaribio la kuipindua serikali ya Zimbabwe
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i34839-mchungaji_apandishwa_kizimbani_kwa_jaribio_la_kuipindua_serikali_ya_zimbabwe
Zimbabwe leo imempandisha kizimbani mchungaji mwanaharakati kwa tuhuma za kujaribu kuipindua serikali; kosa ambalo iwapo atapatikana na hatia adhabu yake ni kifungo cha miaka 20 jela.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Sep 25, 2017 11:42 UTC
  • Mchungaji apandishwa kizimbani kwa jaribio la kuipindua serikali ya Zimbabwe

Zimbabwe leo imempandisha kizimbani mchungaji mwanaharakati kwa tuhuma za kujaribu kuipindua serikali; kosa ambalo iwapo atapatikana na hatia adhabu yake ni kifungo cha miaka 20 jela.

Mchungaji Evan Mawarire anayeongoza harakati kwa jina la "This Flag Movement" anatuhumiwa kuitisha mgomo na malalamiko ya kusalia nyumbani dhidi ya siasa za kiuchumi za Rais Mugabe. Mgomi huo uliofanyika mwaka jana na kushajiishwa kupitia kampeni zilizoendeshwa na mitandao ya kijamii ulikuwa uliwahimiza wananchi kuwasilisha malalamiko yao kuhusu matatizo ya kiuchumi waliyonayo na kushindwa serikali ya Mugabe kuwalipa mshahara wafanyakazi. Mgomo huo umetajwa kuwa mkubwa zaidi kuwahi kuitishwa huko Zimbabwe katika muongo wa hivi karibuni.  

Wafuasi wa mchungaji Evan Mawarire wakiwa nje ya mahakama kuu ya Zimbabwe 

Mawarire alikamatwa tena jana kwa kujaribu kuipindua serikali baada ya polisi kumtuhumu kwamba amekuwa akisambaza taarifa kwa njia za mitandao zinazoituhumu serikali kuwa inaangamiza uchumi wa Zimbabwe. Akiwa ndani ya Mahakama Kuu mjini Harare, mchungaji huyo amekanusha kuwa na hatia kwa tuhuma zilizowasilishwa dhidi yake; makosa mawili yakiwa ya kutaka kuipindua serikali na mawili mengine ya kuchochea machafuko nchini. Chris Mtungadura Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Zimbabwe amesema taarifa zilizotumwa mwaka jana na Mchungaji Mawarire zilikuwa na lengo la kuwachochea wananchi kuipindua serikali. Naye Harrison Nkomo wakili anayemtetea mchungaji huyo amesema kuwa mteja wake alifanya hivyo akistafidi na haki yake ya kikatiba ya kuhoji sera za serikali na kwamba alifanya hivyo kwa kufuata sheria.