Polisi Nigeria wavuruga maombolezo ya Muharram
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i35081-polisi_nigeria_wavuruga_maombolezo_ya_muharram
Polisi nchini Nigeria wamehujumu na kuvuruga maombolezo ya siku za Muharram katika mji wa Sokoto kaskazini mwa nchi hiyo na kuwatia mbaroni Waislamu sita waliokuwa katika maombolezo hayo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 01, 2017 04:19 UTC
  • Polisi Nigeria wavuruga maombolezo ya Muharram

Polisi nchini Nigeria wamehujumu na kuvuruga maombolezo ya siku za Muharram katika mji wa Sokoto kaskazini mwa nchi hiyo na kuwatia mbaroni Waislamu sita waliokuwa katika maombolezo hayo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Harakati ya Kiislamu ya Nigeria IMN, hujuma hiyo imejiri baada ya Kamishna wa Jimbo la Sokoto kupiga marufuku maombolezo ya Mjukuu wa Mtume Muhammad SAW, Imam Hussein AS ambayo hufanyika katika siku 10 za kwanza za mwezi wa Muharram.

Taarifa hiyo imesema pamoja na kuwa mijumuiko na matembezi ya Waislamu katika mwezi wa Muharram huwa ya amani, lakini maafisa wa usalama wamechukua hatua ya kuwahujumu na kuwakamata walioshiriki.

Maandamano ya kutaka Sheikh Zakzaky aachiliwe huru

Wakati huo huo Harakati ya Kiislamu Nigeria imesema itaandaa maandamano mapya ya kutaka kuachiliwa huru kiongozi wa harakati hiyo Sheikh Ibrahim Zakzaky anayeshikiliwa korokoroni pasina kufunguliwa mashtaka tokea Disemba 2015. Maandamano hayo yamepangwa kufanyika katika mji mkuu Abuja.

Itakumbukwa kuwa Sheikh Zakzaky akiwa na mke wake walitekwa nyara na jeshi la Nigeria mwezi Disemba mwaka 2015 katika kituo cha kidini mjini Zaria katika jimbo la Kaduna. Waislamu zaidi ya 1000 waliuliwa na wanajeshi hao wa Nigeria katika tukio hilo.