Machafuko yashtadi Cameroon, Guterres ataka yafanyike mazungumzo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i35209-machafuko_yashtadi_cameroon_guterres_ataka_yafanyike_mazungumzo
Hali ya taharuki na mchafukoge imeripotiwa kushtadi nchini Cameroon huku mashirika ya kutetea haki za binadamu yakivitaka vyombo vya usalama nchini humo kutotumia mbinu za ukatili kuzima malalamiko na maandamano ya wananchi wanaotaka majimbo yao yajitenge na serikali kuu ya Yaounde.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 04, 2017 04:31 UTC
  • Machafuko yashtadi Cameroon, Guterres ataka yafanyike mazungumzo

Hali ya taharuki na mchafukoge imeripotiwa kushtadi nchini Cameroon huku mashirika ya kutetea haki za binadamu yakivitaka vyombo vya usalama nchini humo kutotumia mbinu za ukatili kuzima malalamiko na maandamano ya wananchi wanaotaka majimbo yao yajitenge na serikali kuu ya Yaounde.

Vyombo vya habari nchini humo vimeripoti kuwa mamia ya watu katika majimbo hayo wametiwa mbaroni na maafisa usalama wa nchi hiyo.

Huku hayo yakiarifiwa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amevunja kimya chake na kuizungumzia kwa njia ya moja kwa moja kadhia hiyo. Amesema anaunga mkono mwito uliotolewa na Rais Paul Biya wa nchi hiyo wa kufanyika mazungumzo ya kuupatia ufumbuzi mgogoro huo. 

Maandamano na ghasia Cameroon

Aidha ametoa wito wa kufanyika uchunguzi juu ya mauaji na ukandamizaji unaofanywa na maafisa usalama wa nchi hiyo, dhidi ya waandamanaji, sambamba na kuzitaka pande zote husika katika mgogoro huo zijiepushe na hatua za kuuchochea mgogoro huo.

Hivi karibuni shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International lilitangaza kuwa, kwa akali watu 17 wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa na askari wa jeshi la Cameroon, wakati wa maandamano ya kushinikiza kujitenga maeneo ambayo wakazi wake wanazungumza Kiingereza, katikati mwa nchi hiyo.