Hali ya kibinadamu yazidi kuwa mbaya Sudan Kusini
-
Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini
Gazeti la al Jadid linalochapishwa nchini Uingereza limeandika kuwa, hadi hivi sasa Sudan Kusini imeshindwa kuwa na serikali huru licha ya kupita miaka mingi ya tangu kujitenga na Sudan mwaka 2011.
Gazeti hilo limechapisha makala leo Jumatano na kuandika kuwa, amri iliyotolewa hivi karibuni na Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini ya kuwaamrisha polisi wa nchi hiyo kushirikiana na askari 4000 wa Umoja wa Mataifa watakaotumwa kulinda amani mjini Juba, ni sawa na kukabidhi utawala wa nchi hiyo changa zaidi duniani, mikononi mwa Umoja wa Mataifa.
Kabla ya hapo Umoja wa Mataifa ulikuwa umechukua uamuzi wa kutuma askari 4000 wa kusimamia amani huko Juba, mji mkuu wa Sudan Kusini. Awali serikali ya Juba ilipinga. Hata hivyo sasa hivi Rais Salva Kiir ameruhusu polisi wa nchi hiyo washirikiane na askari hao wa Umoja wa Mataifa,
Gazeti hilo limeongeza kuwa, sasa Rais Salva Kiir anaonekana amebadilisha misimamo na sasa anaelekea upande wa mapatano ya kisiasa. Pia limeandika, hata kama rais huyo wa Sudan Kusini atakubali kujiuzulu kupitia mapatano hayo ya kisiasa, lakini bado hakuna matumaini ya kupatikana amani Sudan Kusini bali lazima yatazuka makundi mengine yatakayopigana vita na serikali.
Gazeti hilo la al Arabi al Jadid limetabiri kwamba, katika siku za usoni, Sudan Kusini itasambaratika na kuundika vijinchi vingine kadhaa hasimu.