Komando wa nne wa Marekani auawa katika hujuma Niger
(last modified Sat, 07 Oct 2017 14:29:44 GMT )
Oct 07, 2017 14:29 UTC
  • Komando wa nne wa Marekani auawa katika hujuma Niger

Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon, imethibitisha kuuawa Komando wa nne wa jeshi la nchi hiyo katika hujuma ya kuvizia nchini Niger ambapo awali ilikuwa imetangazwa ni makomnando watatu waliouawa.

Katika taarifa, Pentagon imesema askari huyo wa nne alikuwa hajulikano aliko na kwamba jana Ijumaa wakaazi wa eneo la tukio waliupata mwili wake.

Itakumbukwa kuwa siku ya Jumatano, shambulizi la kuvizia linaripotiwa kutekelezwa karibu na mji mkuu wa Niger, Niamey ambapo askari hao wane wa Marekani waliangamizwa na wengine kadhaa kujeruhiwa. Taarifa zinasema makomando hao ambao ni maarufu kama Green Berets walifyatuliwa risasi na watu wasiojulikana. Hakuna kundi lolote ambao limedai kuhusika na hujuma hiyo.

Maafisa wa usalama katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi wanasema yamkini hujuma hiyo imetekelezwa na  mtandao wa al-Qaeda wa eneo la Maghreb barani Afrika maarufu kama AQIM.

Maafisa wa Niger wanasema wanaamini waliotekeleza hujuma hiyo waliingia nchini humo kutoka nchi jirani ya Mali.

Ripoti zinasema wanajeshi watano wa Niger ni kati ya waliouawa katika shambulizi hilo ambalo lilijiri wakati askari hao walikuwa katika doria pamoja na makomando hao Wamarekani karibu na mpaka ya Niger na Mali.

Mwezi Mei pia makomando wawili wa Marekani waliuawa katika shambulizi la kundi la kigaidi la Al Shabab nchini Somalia.

Maelfu ya wanajeshi wa Marekani wanaripotiwa kuweko katika nchi kadhaa za Kiafrika katika kile kinachoonekana na jitihada za Washington kutumia kisingizo cha ugaidi kueneza satwa yake ya kijeshi barani Afrika.

 

Tags