Makumi ya watu wenye silaha waangamizwa Algeria
Wizara ya Ulinzi ya Algeria imetangaza kuwa, wanajeshi na polisi wa nchi hiyo wameua magaidi 86 kwenye maeneo tofauti ya nchi hiyo katika kipindi cha miezi minane ya kwanza ya mwaka huu.
Wizara ya Ulinzi ya Algeria ilitangaza habari hiyo jana usiku na kuongeza kuwa, watu wengine laki moja na 26 elfu wametiwa mbaroni katika kipindi hicho kwa tuhuma za kuwa na uhusiano na magenge ya kigaidi.
Operesheni ya karibuni kabisa ya vikosi vya kulinda usalama vya Algeria ni ile iliyofanyika wiki iliyopita ambapo watu sita wenye silaha walitiwa mbaroni katika eneo lililoko umbali wa kilomita 250 mashariki mwa mji mkuu Algiers.
Tarehe 25 Septemba mwaka huu, Waziri Mkuu wa Algeria, Ahmed Ouyahia aliyataka makundi yenye silaha kuweka chini silaha zao ili yanufaike na msamaha uliotolewa na serikali. Vile vile aliwaonya watu wenye silaha kwamba, kama watakataa kuweka chini silaha wajue kuwa imma watauawa au watatiwa mbaroni.
Kijiografia Algeria iko katika eneo ambalo limejaa machafuko. Inapakana na nchi kama Mali na Libya ambazo zina machafuko ya kisiasa na ukosefu mkubwa wa usalama. Ni kwa sababu hiyo ndio maana muda wote Algeria inakabiliwa na hatari za makundi ya kigaidi na magenge ya magendo ya binadamu, ya silaha na ya madawa ya kulevya.