Sudan Kusini yaazimia kutekeleza ahadi ya kusimamisha vita daima
Serikali ya Sudan Kusini imesisitiza tena azma ya kuhakikisha vita vya ndani vinasitishwa nchini humo baada ya kiongozi wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa kutangaza kuwa kukosekana kwa usalama nchini humo kunatokana na ukosefu wa nia ya kisiasa.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo Mawien Makol amesema serikali ya Sudan Kusini itaendelea na juhudi za kutimiza ahadi ya kusimamisha mapambano daima wakati wa mazungumzo kati yake na maofisa wa ngazi ya juu wa Shirika la Maendeleo la Kiserikali ya nchi za Afrika Mashariki (IGAD).
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia ulinzi wa amani Jean-Pierre Lacroix amesema, serikali ya Sudan Kusini bado haijashiriki kikamilifu kwenye mchakato wa amani, ambao unadhaniwa kuwa ni fursa ya mwisho ya kukomesha mgogoro uliodumu kwa miaka minne nchini humo.
Vita vya ndani nchini humo vilivyoanza Disemba 2013 vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. Nchi hiyo ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kuipindua serikali yake.