Nchi jirani na Libya zapinga mashambulizi ya kigeni nchini humo
Mawaziri wa nje wa nchi jirani na Libya wamepinga aina yoyote ya mashambulizi ya nchi za kigeni nchini humo na kuunga mkono serikali mpya ya nchi hiyo.
Katika kikao chao kilichofanyika jana nchini Tunisia, mawaziri wa mambo ya Nje wa nchi jirani na Libya wameunga mkono serikali ya umoja wa kitaifa ya Faiz Siraj na kutangaza kuwa wanapinga mashambuzi yoyote ya nchi za kigeni nchini Libya.
Taarifa iliyotolewa mwishoni mwa kikao hicho cha Tunisia imesisitiza kuwa mgogoro wa Libya imeshika mkondo hatari sana kutokana na kueneza zaidi harakati za kigaidi za kindi la Daesh na kwamba makundi yote ya Libya yanapasa kuungana na kutupilia mbali hitilafu zao kwa ajili ya kupambana na genge hilo la kigaidi.
Kwa upande wake mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya, Martin Kobler ambaye pia amehudhuria mkutano huo amesema kuwa kuwepo kwa wapiganaji wa kundi la kigaidi la Daesh nchini Libya kunahatarisha zaidi hali ya nchi hiyo na kwamba kuna ulazima wa kufanyika jitihada za kukukabiliana na magaidi hao.