Mugabe kutana kwa nyuso za bashasha na wanajeshi; akataa mwito wa kujiuzulu
Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe ambaye anashikiliwa katika kizuizi cha nyumbani kwa mara nyingine tena amekataa mwito wa jeshi unaomtaka ajiuzulu.
Baadhi ya picha zilizoenezwa katika mitandao ya kijamii zinamuonyesha Rais Mugabe akipeana mikono na Constantino Chiwenga mkuu wa majeshi ya nchi hiyo huku wakiwa na nyuso za bashasha na tabasamu baada ya kufanyika mazungumzo kati ya pande mbili. Ripoti zinaeleza kuwa, Rais Mugabe amekataa kabisa mwito unaomtaka ajiuzulu na kuachia ngazi madaraka ya nchi hiyo.
Mugabe amesisitizia msimamo wake huo huku mashinikizo ya kila upande ya kumtaka ajiuzulu wadhifa huo yakiendelea kuongezeka. Kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai alisema mapema kuwa, Mugabe anastahili kujiuzulu mara moja kwa manufaa ya watu na raia wa nchi hiyo.
Siku ya Jumanne wanajeshi wa Zimbabwe walimuondoa madarakani Rais Robert Mugabe wa nchi hiyo kama njia ya kupinga maamuzi yake ya hivi karibuni. Aidha siku hiyo hiyo Mkuu wa Jeshi la Zimbabwe, Constantino Chiwenga alimpa Rais Mugabe muda wa masaa 24 kuhakikisha amemrejesha ofisini makamu wake, Emmerson Mnangagwa, vinginevyo jeshi litangilia kati.
Jeshi la Zimbabwee lilichukua hatua hiyo baada ya Rais Mugabe kumfuta kazi makamu wa Rais Emmerson Mnangagwa, wiki iliyopita, na kuashiria kuwa anapendelea mke wake Grace Mugabe, kuchukua uongozi wa chama cha Zanu-PF na kuwa Rais wa Zimbabwe baada yake.