Chama tawala Zimbabwe chasema hakuna kurudi nyuma, Mugabe ang'atuke
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i36464-chama_tawala_zimbabwe_chasema_hakuna_kurudi_nyuma_mugabe_ang'atuke
Chama tawala nchini Zimbabwe cha Zanu- PF kimetangaza kuwa kinapanga mikakati ya kumlazimisha Rais mkongwe wa nchi hiyo, Robert Mugabe ang'atuke madarakani baada ya kuitawala nchi hiyo kwa kipindi cha miaka 37.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Nov 17, 2017 13:21 UTC
  • Chama tawala Zimbabwe chasema hakuna kurudi nyuma, Mugabe ang'atuke

Chama tawala nchini Zimbabwe cha Zanu- PF kimetangaza kuwa kinapanga mikakati ya kumlazimisha Rais mkongwe wa nchi hiyo, Robert Mugabe ang'atuke madarakani baada ya kuitawala nchi hiyo kwa kipindi cha miaka 37.

Maafisa wa chama cha ZANU-PF wanasema wanataka Mugabe aondoke madarakani la sivyo chama kitamlazimisha kung'atuka.

Maafsa hao wamesema" "Ikiwa Mugabe atakuwa mkaidi na kung'ang'ania madaraka, chama kitatayarisha mazingira ya kumfukuza Jumapili ijayo na wakati huo ataitwa na kusailiwa siku ya Jumanne."

Afisa mmoja wa chama tawala cha Zanu-PF amesema: Hakuna kurudi nyuma na hali ya sasa nchini ni sawa na mechi ya soka iliyocheleweshwa kwa mvua kali huku timu ya nyumbani ikiongoza kwa magoli 90 kwa sifuri katika dakika ya 89."  

Mugabe katika sherehe za kuhitimu wanafunzi wa chuo kikuu, Harare

Wakati huo huo jeshi la Zimbabwe linamtaka Rais Robert Mugabe wa nchi hiyo aondoke madarakani kwa amani na kuruhusu serikali ya mpito chini ya uongozi wa aliyekuwa makamu wake, Emmerson Mnangagwa, ambaye alimtimua kazi wiki iliyopita.

Lengo la hatua hiyo ya jeshi ambalo linashikilia madaraka kwa sasa ni kuzuia jario la aina yoyote la Robert Mugabe la kumkabidhi madaraka mkewe, Grace Mugabe.

Kiongozi huyo ameonekana hadharani kwa mara ya kwanza leo katika sherehe za kuhitimu masomo wanafunzi wa chuo kikuu mjini Harare tangu jeshi la Zimbabwe lilipotwaa madaraka ya nchi siku kadhaa zilizopita.

Jeshi la Zimbabwe linadhibiti maeneo muhimu ya nchi hiyo

Wachambuzi wa mambo wanasema Mugabe anajaribu kuchelewesha suala la kung'atuka kwake madarakani hadi wakati wa uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika mwakani.