Muswada wa kumsaili Mugabe, wawasilishwa katika bunge la Zimbabwe
Mpango wa kusailiwa Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe umewasilishwa katika bunge la nchi hiyo.
Habari kutoka Harare, mji mkuu wa Zimbabwe zinasema kuwa, Jumamosi ya jana chama cha upinzani kiliwasilisha mpango huo bungeni, kikitaka Mugabe asailiwe ndani ya bunge hilo. Hii ni katika hali ambayo kabla ya hapo chama tawala nchini humo cha Zanu-PF sambamba na kupitisha muswada wa kutokuwa na imani na Mugabe katika mkutano wa chama hicho, kilitangaza kuwa kinaandaa mpango wa kumvua madaraka kiongozi huyo na kukabidhi madaraka hayo katka mkutano ujao.
Jumatano iliyopita ya tarehe 15 Novemba, jeshi la Zimbabwe lilichukua udhibiti wa nchi sambamba na kumuweka kizuizini Rais Mugabe, huku likikanusha kufanya mapinduzi ya kijeshi. Wakati huo huo, maelfu ya raia waliandamana jana nchini humo hasa katika mji mkuu Harare wakiunga mkono hatua ya jeshi ya kutaka kumuondoa madarakani Rais Robert Mugabe na kupiga nara wakishinikiza kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 93 ajiuzulu haraka na kuachia madaraka ya nchi.