Rais wa Cameroon awaonya watu wenye silaha
Rais Paul Biya wa Cameroon amewaonya watu wenye silaha wanaopigania kujitenga maeneo ya nchi hiyo yanayozungumza Kiingereza.
Paul Biya ametoa onyo hilo jana Ijumaa na kusisitiza kuwa, nchi yake imekuwa muhanga wa mashambulizi ya mara kwa mara ya watu wanaotaka kujitenga. Amesema, watu wanaotaka kujitenga ni tishio kwa usalama wa nchi yake kwani katika kipindi cha wiki moja iliyopita, wameua wanajeshi wanne na askari polisi wawili.
Rais wa Cameroon amesema hayo wakati aliporejea nchini humo akitokea Kodivaa alikoshiriki kikao cha viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya na nchi za Afrika.
Cameroon
Makumi ya raia wameuawa tangu mwezi Oktoba hadi hivi sasa kutokana na machafuko yaliyozuka baina ya vikosi vya serikali na wapinzani katika maeneo yanayozungumza Kiingereza nchini Cameroon.
Idadi kubwa ya raia wa Cameroon wanazungumza Kifaransa hata hivyo idadi ya wanaozungumza Kiingereza si ndogo. Inadaiwa kuna asilimia arubaini ya wazungumzaji wa Kiingereza nchini Cameroon. Maeneo hayo yanayozungumza Kiingereza yanalalamika kuwa yamepuuzwa na yametengwa na serikali ya nchi hiyo.
Ukandamizaji unaofanywa na serikali ya Cameroon katika maeneo hayo umewalazimisha wakazi wake kuunda makundi ya kujitenga. Makundi hayo yameshadidisha mashambulizi yake hivi sasa ambapo Cameroon inajiandaa kwa ajili ya uchaguzi wa Rais mwakani.