AU na EU zataka kutatuliwa mgogoro wa wahajiri wa Kiafrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i37075-au_na_eu_zataka_kutatuliwa_mgogoro_wa_wahajiri_wa_kiafrika
Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya zimetilia mkazo udharura wa kutafutwa ufumbuzi wa kimsingi wa hali mbaya ya wakimbizi na wahajiri wa Kiafrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 02, 2017 05:00 UTC
  • AU na EU zataka kutatuliwa mgogoro wa wahajiri wa Kiafrika

Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya zimetilia mkazo udharura wa kutafutwa ufumbuzi wa kimsingi wa hali mbaya ya wakimbizi na wahajiri wa Kiafrika.

Hayo yamesisitizwa katika taarifa ya mwisho mkutano wa 5 wa viongozi wa Afrika na Ulaya uliomalizika jana mjini Abidjan nchini Ivory Coast. Taarifa hiyo imesema kuwa, suala la wakimbizi na wahajiri wa Kiafrika linapaswa kupatiwa ufumbuzi wa kimsingi ikiwa ni pamoja na kupatikana suluhisho la kisiasa la mgogoro wa Libya. 

Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya pia zimelaani mienendo ya kinyama ya makundi ya wahalifu dhidi ya wahajiri na wakimbizi wa Kiafrika na kutangaza azma yao kubwa ya kushirikiana kwa ajili ya kukomesha haraka uhalifu huo na kuboresha hali ya wakimbizi.

Wahajiri wa Kiafrika, Libya

Pande hizo mbili pia zimetilia mkazo udharura wa kuboreshwa hali ya wakimbizi nchini Libya na kuwasaidia kurejea katika nchi zao. 

Itakumbukwa kuwa hivi karibuni zilienea picha na filamu kwenye mitandao ya kijamii zilizoonyesha raia wa nchi za Kiafrika wanaohajiri kuelekea Ulaya wakiuzwa kama watumwa nchini Libya.